MWASIMA MBUWA WELFARE NI TAPELI SUGU

Katibu Mkuu wa Mwasima Mbuwa Welfare Society Bw. Mwaluma Mnjala

Na Mwandishi wa Kwaela News Network

Ni wazi kwamba ardhi ni moja ya rasilmali kuu za uzalishaji mahali popote duniani. Hivyo basi ilikuwa ni furaha yangu kuu asubuhi ya leo, kusikia kupitia kwa chombo kimoja cha habari ya kwamba wananchi wa Majengo Singila, eneo la Mwatate, watamiliki ekari takriban mia mbili na hamsini kutoka kwa shamba la makonge la Teita Estates Ltd. Ripoti hiyo ni sawia na semi ambazo Waziri wa Ardhi wa Kaunti ya Taita Taveta, Ndugu Mwandawiro Mghanga, alizitoa katika studio za Anguo FM yapata kama mwezi mmoja uliopita sasa. Isitoshe, Mwandawiro aliongeza kusema kwamba eneo lengine la takriban ekari mia tatu, zimetengwa kutoka kwa shamba hilo hilo lamakonge, kwa manufaa ya wananchi wa Landi.

KIU YA MASHAMBA

Umiliki wa ardhi hiyo, hasa kwa wananchi wa Singila Majengo, ni ushindi mkubwa kwao, hasa ukitilia maanani ya kwamba waliungana chini ya “SINGILA MAJENGO GROUP” kutetea ardhi hito katika kesi ambayo iliamuliwa tarehe 11 Mei mwaka wa 2011.

Kwa kuwa ongezeko la watu limeleta presha ya umiliki wa ardhi, hasa katika maeneo ya milimani, watu wengi hukimbilia mahali popote wasikiapo ya kuwa kuna ardhi inauzwa, au kugawanywa. Kiu hii ya ardhi ndio ilipelekea jamaa fulani kuungana na kuunda kikundi cha “Welfare Group” ambacho wamekuwa wakihadaa wananchi kwamba “watawagawanyia maelfu na maelfu ya ekari ambazo zilinyakuliwa na shamba la Teita Estates”. Hata ingawa “Welfare Groups” haziruhusiwi kuingilia maswala ya uwekezaji na ununuzi wa ardhi, kundi hilo lilijisajili kwa jina la MWASIMA MBUWA WELFARE SOCIETY. 

Ajabu ni kwamba viongozi wa kundi hilo la Mwasima Mbuwa Welfare Society, ambalo wananchi wa Taita Taveta wamelichangia mamilioni ya pesa kwa miaka zaidi ya kumi kufikia sasa, wamegeuka kuwa mabubu, wasiseme lolote kuhusu hatima ya ardhi hii iliyotolewa kwa wananchi. Hawataki kusema ukweli ya kwamba ARDHI HIYO IMETOLEWA KWA WAKAZI WA SINGILA MAJENGO – na haitafaidi wananchi wote wale waliotapeliwa na Mwasima Mbuwa. Badala yake, kila “wanahisa” wanapopiga simu, wanazidi kuhimizwa kutoa hela zaidi “ili kupata ekari kubwa zaidi wakati wa mgao” na vile vile, kushurutishwa waongeze hela zengine “kama gharama za kumlipa wakili wetu”.

MASWALI KWA MWASIMA MBUWA

Swali la kwanza ni : kwa nini wananchi waendelee kutoa pesa kwa wakili wakati tayari koti iliamua kitambo sana (Mei 11, 2011) ya kwamba ardhi yote ya shamba la Teita Estates ipimwe na MASOROVEYA KUTOKA PANDE ZOTE HUSIKA ili ibainishwe ikiwa ni kweli shamba hilo la makonge  limenyakua eneo zaidi ya ekari elfu thelathini, ambazo ndio inazomiliki kihalali. Matokeo ya usoroveya huo ulibainisha ya kwamba shamba hilo limekalia eneo ya ekari 30,284.

Swali lengine :  “Ni nini hatima ya mamilioni yote wananchi walitoa kwa kununua shamba ambalo ni wazi sasa ya kwamba ni “shamba hewa” lililoahidiwa na watapeli hawa?

MAJONZI

Inasikitisha sana kusikia vile waliotapeliwa na genge hilo wanapitia mateso makubwa kwa hasara waliyopata. Wengine waliaga dunia kwa sababu ya magonjwa kama presha na “depression”. Wengine wanalipa loni walizokopa, wengine wakauza mifugo yao…..na hadi sasa, baada ya miaka zaidi ya kumi kumi, bado wanazidi kushurutishwa waongeze pesa zaidi! Majonzi haya si kwa watu binafsi pekee : kupitia kwa bwenyenye mmoja anayefanya biashara zake Mombasa, hata makampuni mengi na vyama vingi vya ushirika viliweza kushawishiwa na kuingiza mamilioni kwenye kashfa hii ambayo imeelekea kutajirisha bwenyenye huyo na viongozi wa Mwasima Mbuwa Welfare. Isitoshe, bwenyenye huyo hakukomea hapo : alishawishi makanisa mengi “kuwekeza” rasilmali zao vile vile. Sasa waliotapeliwa wamejikuta kwenye njia panda – utaendaje kuombewa kwa hasara uliyopata ilhali kanisa hilo hilo unaenda kuombewa pia limetapeliwa?

KURUDISHIWA FIDIA

Siku za hivi majuzi, tangu Mwandawiro Mghanga kufichua ukweli wa mambo, watu wengi wamejua kuwa pesa zao zimeliwa na wajanja. Katika ofisi za Mwasima Mbuwa pamoja na Bweyenye huyo wa Mombasa, imekuwa hali ya “mwenye nguvu mpishe”. Wale walio na uwezo wa kushtaki matapeli hao ndio wanaorudishiwa pesa zao kwa njia ya siri. Maskini walala hoi – kama ilivyo kawaida – ndio wanaachwa wapambane na hali zao.

Ombi langu ni hili : Mwasima Mbuwa warudishie watu wote pesa zao BILA YA KUBAGUA. Lau sivyo waliotapeliwa wataungana na kuwashtaki wahusika wote waliowatapeli.

more recommended stories