RUTO AHITIMISHA ZIARA YAKE PWANI HUKU CHECHE KALI ZA SIASA ZIKIENDELEA KUSHUHUDIWA

Makamu wa Rais William Ruto akitiliwa chai na mkaazi wa Taita Taveta

Naibu wa rais William Ruto amewakosoa baadhi ya viongozi wa upinzani wanaoingilia vita dhidi ya ufisadi na kuwataja kama wasiotambua majukumu yao kikatiba huku akiomba tume huru ikiwemo mahakama kupewa uhuru wao kutekeleza yale yanayowahusu bila kuingiza siasa.

Akiongea kaunti ya Taita Taveta alipotamatisha ziara yake ukanda wa Pwani, Ruto ameutaja upinzani kama uliochanganyikiwa huku akihoji kuwa suluhu la ufisadi nchini ni kuruhusu tume huru kutekeleza majukumu yao na wanasiasa kusalia na agenda za maendeleo na sio kujikanganya.

“Wasjifanye wao ndio wanapigana na vita dhidi ya ufisadi. Katiba iko wazi kuhusu nani mwenye mamlaka ya kuongoza vita hivi. Tutaunga mkono tume zilizotwikwa majukumu kupigana na vita hivyo. Kama huna agenda ya maendeleo wacha kuingiza siasa kwa maswala ya ufisadi.” Ruto amesema

Amesema atazidi kushiriki michango ya kufanikisha maendeleo licha ya pingamizi kutoka kwa wapinzani wake, na kuomba walio na tashwishi kuhusu fedha alizonazo kueleza wakenya pale wanapopeleka fedha zao.

“Wawache fitina na hawawezi kunitisha. Viongozi wetu wa kidini msiwe na wasiwasi kwa kua ntazidi kuunga mkono ujenzi wa makanisa kupitia raslimali zangu binafsi.” Ametoa hakikisho.



Swala la siasa pia limepenyeza huku akisema mpango alionao ni kuleta viongozi pamoja kufanikisha agenda 4 kuu za serikali na sio vuguvugu la kisiasa kama inavyosemekana na wapinzani wake.

“Wale wanaongea mambo mengi ju ya William Ruto nawammbiwa kua ni debe tupu ndizo huongea kuhusu wenzao. Kama wanashida nikiungana na wajumbe wa pwani nikifanya maendeleo nataka niwaambie sina muda na wao ila kutumikia wakenya.” Ameongeza

Ruto aliandamana na viongozi wa kisiasa ikiwemo gavana Granton Samboja ambapo wamezindua miradi kadha kaunti hiyo ikiwemo Huduma za CT – Scan hospitali ya rufaa ya Moi mjini Voi, mradi wa maji Mbulia na ule wa nguvu za umeme ‘Last Mile’ wa kima cha shilingi milioni 520 mjini Wundanyi huku akiongoza michango miwili kanisa la Pefa mjini Voi na mwingine shule ya upili ya Dr. Aggrey mjini Wundanyi.

Gavana samboja kwa upande wake ameahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya kitaifa ili kufanikisha maendeleo kaunti yake na kuomba wananchi kujiepusha na siasa ya kuligawanya taifa, hoja iliyoungwa mkono na wajumbe Naomi Shaban (Taveta), Jones Mlolwa (Voi) na Danson Mwashako (Wundanyi).

“La muhimu ni sisi wote kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikiwa kupata maendeleo. Hatutafanya siasa ya upofu ila ya maono na maendeleo. Ni vyema pia tushirikiane na wajumbe wa kaunti kuhakikisha tunafanikisha agenda kuu za serikali ya kitaifa.” Kwa kauli moja wamesema.

more recommended stories