Katika wakati ambapo wananchi wa Taita Taveta wanahangaika na umasikini, ukosefu wa maji, barabara mbovu, miradi iliyokwama na bili ambazo bado hazijalipwa, ni jambo la kusikitisha, la kuudhi na la kuaibisha kuona baadhi ya viongozi wetu wakisaka safari ya kifahari kwenda Paris nchini Ufaransa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 22.
Ni vigumu kuelewa ni kwa nini Spika Wisdom Mwamburi, Hon. Tondoo wa Bomeni, Hon. Azar wa Kaloleni, Hon. Mlughu wa Rong’e, Hon. Taraya wa Mboghoni, Hon. Joseph “Anko” wa Mwatate na wengineo wanaonekana kuwa na haraka kubwa ya kusafiri kwenda Paris kuandamana na kundi la wacheza ngoma wa MWAZINDIKA wakati wananchi wao wanaishi katika hali ya kukata tamaa.
Je, hii ndiyo ile siasa ya “wakati wetu wa kula”? Je, viongozi hawa wanaamini kuwa hazina ya kaunti ipo kwa ajili ya starehe zao binafsi na matembezi ya nje ya nchi? Inasikitisha kuona kwamba ni mwezi mmoja tu kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha, badala ya fedha hizo kuelekezwa kwenye miradi ya dharura, madeni ya wakandarasi, huduma za afya au maji, baadhi ya viongozi wanaonekana kutokwa na mate kwa safari ya kifahari ya Ulaya.
Read Also; PARIS ON OUR PAIN: TAITA TAVETA MCAs STILL FEEDING WHILE THE COUNTY BLEEDS
MWAZINDIKA ni kikundi cha ngoma za asili za Kitaita kinachopatikana hapa hapa nyumbani. Kwa kweli, je, tunahitaji kutumia milioni 22 ili MCAs waone ngoma hizo Paris? Kama ni kutazama utamaduni wetu, si ingewezekana kabisa kuandaa maonesho hayo katika viwanja vya assembly kwa gharama ya chini ya shilingi elfu kumi? Hata kundi la URUASI kutoka Taveta lingeweza kushiriki kwa heshima na usawa.
Lakini hapa ndipo swali la uchungu linapoanzia. Kwa nini MWAZINDIKA wamekuwa wakipelekwa India juzi na sasa Paris, huku URUASI hawajawahi hata kupewa nafasi? Kwa nini viongozi kutoka Taveta kama Hon. Taraya na Hon. Tondoo hawaulizi kuhusu ubaguzi huu wa wazi? Je, utamaduni wa Taveta si sehemu ya Taita Taveta?
Kinachoumiza zaidi ni kwamba hata baada ya wananchi kupaza sauti kupitia mitandao ya kijamii, viongozi hawa bado wanadaiwa kusema kuwa “kelele za social media” hazitawazuia kusukuma safari hiyo kwa nguvu. Inasemekana kuwa Gavana lazima aidhinishe safari hiyo “la sivyo kutakuwa na madhara” — kama si sasa basi baadaye. Kauli kama hizi zinaonyesha siyo tu kiburi cha mamlaka, bali pia siasa za vitisho dhidi ya uongozi wa kaunti. Hii ni dharau ya kiwango cha juu kwa wananchi waliowachagua. Ni ishara ya viongozi walioanza kuona wananchi kama watu wa kawaida wasiostahili kusikilizwa.
Wakati huo huo, CECM wa Biashara na Utamaduni, Hon. Gertrude Shuwe, anaripotiwa kufadhaika kwa sababu hakuna fedha za safari hiyo. Lakini bado shilingi laki sita zinatarajiwa kutolewa leo tarehe 8 Mei 2026 na upande wa Executive kwa ajili ya VISA processing. Hii ni katika kaunti ambayo wananchi wengi hawawezi hata kumudu karo ya watoto wao, dawa hospitalini au chakula cha siku.
Taita Taveta inaonekana kama kaunti iliyolaaniwa na uongozi unaopenda safari kuliko huduma, starehe kuliko maendeleo, na sifa za nje kuliko kilio cha wananchi wake. Kila mwaka ni hadithi ile ile: viongozi wachache wakinufaika huku wananchi wengi wakizama kwenye umasikini.
Wananchi wanapaswa kujiuliza: mpaka lini tutaendelea kutawaliwa na viongozi wanaojiona kama mabwana wetu badala ya watumishi wetu? Mpaka lini fedha za umma zitaendelea kutumiwa kama zawadi ya kisiasa kwa wachache wenye mamlaka?
Safari ya Paris si kipaumbele cha mwananchi wa Taita Taveta. Kipaumbele ni maji, afya, ajira, elimu, barabara na kulipwa kwa pending bills. Viongozi wanaoshindwa kuelewa hilo wamepoteza mwelekeo wa uongozi wa umma.
Mungu aiokoe Taita Taveta kutoka kwa viongozi wasio na hisia kwa mateso ya wananchi wao.
By Kwaela News Network (KNN) | Governance & Accountability The seven-day ultimatum issued to…
The days when political party waves and symbolism single-handedly determined election outcomes in Taita-Taveta…
The growing controversy surrounding the financial management of Taita Taveta County has taken another…
Perhaps one of the most ironic moments of Governor Andrew Mwadime's appearance before the…
Affected families in Mlambenyi, Golani and Mto Mwagodi face a February 2027 deadline as the…
During a Senate Public Finance Committee meeting, Taita Taveta Governor Andrew Mwadime, popularly known as…
Leave a Comment