WAPWANI HATUUNGANI

 

Hakuna aletulani, wapwani twatukanishwa

Si viongozi fulani, ni sera inahuishwa

Tafauti ziko ndani, ubaguzi wadumishwa

Wapwani hatuungani, hata tukiunganishwa

Dharau zetu wapwani, twaridhi kugawanyishwa

Kwa sauti za puani, matabaka yavumishwa

Kwani yule ajuani, kila mtu apimishwa

Wapwani hatuungani, hata lau twagandishwa

Unasema kama nani, na wewe hujaapishwa

Wapwani tuvisirani, nyongo hatujatapishwa

Hatuna na hatunani, ndiposa tunateteshwa

Wapwani hatuungani, kwa sababu twaendeshwa

Daima hatupatani, wasemao wanatishwa

Ni mipango ya zamani, dhaifu kudhalilishwa

Twajigawanya kidini, na wenyewe twaridhishwa

Wapwani hatuungani, nyoyo hazijasafishwa

Kuna hujuma fulani, ambayo inafanishwa

Visu vyetu vi alani, vyao vinameremeshwa

Tunatindwa uwandani, na sisi twafurahishwa

Wapwani hatuungani, twazidi kukorofishwa

Pwani hatukiriani, umoja unafurushwa

Tunalishwa biriani, twanunuliwa kwa rushwa

Wapwani fikiriani, mbona twazidi kurushwa

Wapwani hatuungani, wafuasi twachokeshwa

Hata tukafanywa nini, ari yetu itafishwa

Twajulikanwa yakini, ndipo tukadhoofishwa

Tuna vifuta nyoyoni, haturidhi kufifishwa

Wapwani hatuungani, vyetu vinatilifishwa

Mohamed Khamis

Takaungu”

04.05.2021

 

 

 

 

 

 

 

 

more recommended stories