HOTUBA YA GAVANA GRANTON SAMBOJA, WAKATI WA KUADHIMISHA SHEREHE ZA MASHUJAA TAREHE 20, OKTOBA 2020, KATIKA UWANJA WA SHULE YA UPILI YA MWATATE.

Naibu Gavana,

Kamishna wa Kaunti hii na maafisaa wa vitengo vya usalama kaunti hii,

Mhe. Seneta , Kaunti ya Taita Taveta,

Waheshimiwa wa bunge letu la kitaifa,

Spika wa bunge letu la kaunti,

Wawakilishi wadi,

Mawaziri wa kaunti hii pamoja na wafanyikazi wa kaunti yetu ya Taita Taveta,

Viongiozi wa kidini na wale wa matabaka mbalimbali,

Wananchi wa kaunti hii,

Nikizingatia itifaki zote…

Mabibi na Mabwana Hamjambo?

Leo tunasherehekea siku ya Mashujaa tukikumbuka muanzilishi wa taifa letu la Kenya na wazalendo wengine waliojitolea muhanga kukomboa taifa ili tuzidi kusherehekea matunda ya UHURU.

Hatuwezi kusahau mateso waliyopitia Mashujaa wetu ambao waliteswa na mabeberu, wengine wakafungwa jela na hata kuuwawa ili tuwe na UHURU ambao tunajivunia.

Kati ya faida kubwa tuliopata kupitia katiba ya 2010 ni UGATUZI ambao kwa hivi sasa tuko katika awamu ya pili. Ningependa tena kuwashukuru wananchi wote kwa kunipa fursa hii kuwaongoza kama gavana wa pili wa kaunti ya Taita Taveta.

Kwa kunichagua ili kuwatumikia, nyinyi ni MASHUJAA wangu.

Wananchi wapendwa

Ni wazi kwamba safari hii ya miaka mitatu haijakosa changamoto zake, sio kwetu tu bali ulimwenguni kote. Janga la korona limetuathiri kiuchumi, kiafya na sekta mbalimbali. Janga hili lisilo la kawaida limepelekea dunia nzima kusitisha miradi kadha ya maendeleo kuruhusu fedha kuelekezwa katika mikakati ya kulinda afya za wanadamu wote.

Watu wengi wamepoteza ajira, Biashara nyingi zimeathirika na watu kupoteza maisha. Kaunti hii vilevile haijasazwa na ndiposa tunazidi kuweka mikakati kuhakikisha tunapambana na utandavu huu.

Kwa kufanikisha vita hivi, serikali yangu imejenga chumba maalum kitakacho stiri vitanda mia moja na sitini(160 beds) kwenye . hospitali kuu ya Mwatate. Hivi karibuni tutageuza sehemu hiyo kuweko na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) pamoja na HDU.

Leo hii nachukua fursa hii kuwataja wahudumu wa idara ya afya kama mashujaa ambao wamekua mstari wa mbele kukabiliana na janga hili hatari. Pia, tunatambua vitengo vya ulinzi na idara zote husika kwa mchango wenu katika kufanikisha vita dhidi ya ugonjwa huu hatari.

Ili tuwe mashujaa, ni muhimu tuzidi kuzifuata taratibu na kanuni za shirika la afya ulimwenguni WHO na wizara ya afya nchini ambazo ni pamoja na kuvaa barakoa, kuzingatia usafi na umbali wa angalau mita moja.

Mabibi na Mabwana

Tukisalia kwenye sekta hii muhimu ya afya,

Hivi majuzi tu tulizindua kituo cha matibabu na udhibiti wa ugonjwa wa SARATANI katika hospitali ya Rufaa ya MOI Mjini Voi. Hatua hii kwa pakubwa italeta afueni kwa waathiriwa ambao wamekua wakisaka huduma hizo inje ya kaunti hii kwa kulazimika kusafiri hadi kaunti za MOMBASA na NAIROBI.

Tangu kufunguliwa kwake, kituo hicho kimefanikiwa kuwapima takriban watu 251, 45 kati yao wanaendelea kupata matibabu kutoka kwa wataalam wetu wa afya.

Pia tumezindua kliniki ya kushuhulikia saratani ya damu (sickle cell and hemophilia) katika hospitali ya Rufaa ya Moi na hospitali kuu ya Taveta.

Vile vile tulianzisha huduma ya matibabu ya nje (OUTPATIENT CLINIC) hospitali ya Moi mjini Voi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika zahanati hiyo kama njia moja ya kuboresha huduma ya Afya.

Ili kuboresha utoaji huduma za afya nyanjani, tumezindua zahanati kama vile George Faraji, Vighombonyi na pia kuongezea wadi ya wanaume katika kituo cha afya cha Mbale.

Mipango ya kukamilisha ujenzi wa zahanati za Kachero, Malukiloriti, Zungulukani, Kamtonga, Shigharo, Paranga, na Lumi zimezidi kushika kasi na hivi karibuni zitazinduliwa rasmi.

IDARA YA MAJI

Kama nilivyokuwa nimeahidi kuleta maji safi na yanayotiririka kwa kila boma, tayari safari hiyo imeng’oa nanga.

Kwa ushirikiano na Benki kuu ya Ulimwengu, serikali yangu imeanzisha mikakati ya kuboresha mradi wa maji wa NYANGORO utakao sambaza bidhaa hiyo kwa wananchi wa MAKTAU, GODOMA, KWA MNENGWA, KWA NDOTO, MWASHUMA, MWAMBOTA, OVERSEAR NA MWASHOTI na nyanda za chini. Mradi huu unatarajiwa kutosheleza mahitaji ya jamii ya yatu takriban elfu kumi na saba (17,000 people).

Kwa ushirikiano wetu na Benki hiyo, mpango wa kusambaza maji kutoka kituo kikuu cha KARIOKOR mjini Voi kuelekea kwenye tangi la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita million sita ya maji chuo kikuu cha Taita Taveta, Mariweni unaendelea.

Maji hayo yatawafikia wakaaji wa Mariwenyi, Shelemba, Mengo, Landi, Sisera, hadi Chakaleri kabla ya kuelekezwa miji yetu Mikuu ya Voi, Wundanyi, Taveta na Mwatate kwa siku zijazo. Tumeekeza kwa mabomba ya kisasa ya maji kwa kima cha shilling million Themanini ambayo yatatumika kuimirisha miundo misingi ya miradi ya maji ili kuboresha usambazaji wa bidhaa hii imekua adimu kwa mikaka.

MABIBI NA MABWANA

IDARA YA KILIMO

Kama munavyo fahamu kilimo ndio uti wa mgongo wa sehemu kubwa ya Maisha yetu huku. Hivyo basi serikali yangu imetia kila jitihada kuwezesha ukuwaji wa kilimo mambo leo na mbinu mpya za kukuza ukulima wa faida kwa jamii.

Kwa muda usiokuwa mrefu tutakamilisha na kufungua milango kwa wakulima wa ndizi huko Taveta tutakapo kamilisha kiwanda cha kuongeza faida kwa zao hilo. Hii itakuwa afueni kubwa hasa ukifahamu kuwa mkulima wa zao la ndizi amekuwa akinyanyaswa sana na wafanyi Biashara walagai ambao hujifaidisha wenyewe na kumuwacha mkulima hali duni.

Pia tusisahau magari 4 yalionunuliwa na serikali yangu, mawili ya kusambaza maji safi na mawili ya kuzoa maji taka. Hii itasaidia kuboresha utoaji huduma kwa wananchi wangu.

WANANCHI WENZANGU,

SEKTA YA BARABARA

Serikali yangu imeendelea kupanua Barabara zinazo unganisha masoko na wakulima wetu nyanjani pamoja na kubuni Barabara mpya vinazoweza kustahamili mabadiliko ya hali ya hewa.

NIKIMALIZIA,

Mabibi na mabwana

Ni vyema pia kutambua mashujaa wengine wa kitaifa hasa viongozi wetu Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu nchini Raila Odinga kwa kushikana mikono na kuleta amani nchini Kenya wakati nchi ilipokuwa na ati ati baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2017.

Umoja wa mashujaa hao wawili kwa sasa umetuletea ripoti ya BBI ambayo inatarajiwa kufanikisha ugatuzi nchini kwa kuongeza mgao wa Kaunti zetu kwa asilimia 45. Hii itasaidia kuboresha zaidi sekta muhimu kama vile MAJI, ELIMU, AFYA, BARABARA ambazo bado zinazidi kushuhudia changamoto mbalimbali.

Wananchi wa Taita na Taveta napenda sana kuwakumbusha kwamba NYINYI NDIO MASHUJAA WANGU na mimi na serikali yangu NITAWATUMIKIA KWA HALI NA MALI.

YOSHUA 1:6

Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa.

ASANTENI NA MUNGU AWABARIKI NA AIBARIKI KENYA YETU.

Happy Mashujaa Day!

H.E GRANTON GRAHAM SAMBOJA

GOVERNOR

more recommended stories