Categories: Voice of Reason

MWACHERE SHUMA: KIOO CHA UKWELI?

Hivi majuzi, Gavana Wakujaa alimpa mwana blogu Mwachere Shuma kipigo cha maneno akimtuhumu kwa kuandika porojo.

Gavana alimshutumu vikali, akidai kuwa Mwachere huwakosoa watu kwa sura zao, haswa wale wenye “sura za kipombe pombe.” Gavana Wakujaa alionekana mwenye hasira sana, huku maneno yakimkwama kinywani kwa hasira.

Lakini je, kweli Mwachere haelewi anachoandika?

Wakujaa na mwana blogu huyu wana historia. Gavana alidai kuwa mwana blogu huyo alianza kumkosoa tangu akiwa mbunge wa Mwatate.

Hii ni kweli. Miaka kadhaa iliyopita, Mwachere alifichua miradi mbalimbali iliyokwama katika eneo bunge la Mwatate, kama vile Shule ya Sekondari ya Laghonyi, Barabara ya Godoma Manjiwu, Barabara ya Bura Mission – Mrughua – Mghange, na madarasa chakavu ya Mnamu – Mrughua – Mwavunyu.

Hii ni mifano michache tu, na mingi zaidi iliwekwa wazi hapo awali.

Aidha, Wakujaa alipoingia madarakani kama Gavana, alitoa ahadi kibao, ambazo nyingi zimeishia kwenye kapu la sahau. Hii imempa Mwachere nafasi ya kuendelea na kazi yake ya kukosoa na kuangazia udhaifu wa uongozi wa Gavana na hivyo kuibua maswali mazito kuhusu utendakazi wa serikali yake.

Hebu tuchambue baadhi ya masuala ambayo mwana blogu huyo ameyaangazia:

1. Mikopo ya HELB: Aliibua swali la makato ya Helb ya kaunti kutoka kwa mishahara ya watu licha yao kutofaidika kwa mikopo hiyo. Wakujaa hajazungumzia jambo hili. Pia, hakuna aliyekamatwa kwa wizi huu.

2. Bwawa la Kishenyi: Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Wakujaa alidai kutumia Sh85M kusafisha bwawa hili. Hadi leo, hakuna anayejua pesa hizo zilitumika lini na kwa nini.

3. Fidia ya Wanyamapori: Wakujaa aliahidi fidia kwa walioathiriwa na wanyamapori. Miaka miwili imepita, na hakuna aliyepata fidia.

4. Ambulensi ya Taveta: Wakujaa alishangazwa na swali hili. Ukweli ni kuwa hakuna anayejua ni kiasi gani cha pesa kilitumika kununua ambulensi hiyo “mpya.” Bajeti inaonyesha ilitengewa Sh12M. Hiyo ndiyo bei yake au kuna mengine?

5. Uajiri wa Walimu wa Chekechea: Mwaka 2023, serikali ya Wakujaa ilitangaza nafasi za kazi za walimu wa chekechea. Baada ya maombi na mahojiano, bunge la kaunti lilisitisha uajiri kwa siku 90 kutokana na bajeti kubwa ya mishahara ya wafanyakazi. Je, hizo siku 90 hazijawahi kuisha hadi leo?

6. Makato ya Kisheria (Statutory Deductions): Mgomo wa wahudumu wa afya ulifichua mambo ya kushangaza. Ripoti ya makubaliano kati ya serikali ya kaunti na wahudumu ilionyesha kuwa serikali haikuwa ikipeleka makato hayo kwenye taasisi husika, ingawa serikali kuu ilikuwa inatoa mgao huo kwa kaunti. Serikali pia ilikuwa na deni la mishahara, bima, na madeni mengine. Pesa hizo zilikuwa zinaenda wapi?

La kushangaza, wahusika wakuu walipobainika, Gavana aliwahamisha idara nyingine badala ya kuwachunguza na kuwashtaki. Hii inaonyesha wazi kuwa vita dhidi ya ufisadi ni “hadithi za Abunwasi.” Wakujaa hana nia ya kupambana na ufisadi.

7. Mfuko wa Basari: Mwaka jana, kulikuwa na suala la hundi za busari zilizokataliwa. Wanafunzi walirudishwa nyumbani kwa sababu cheki zao zilikuwa “feki.” Hakuna aliyechukua lawama. Ilikuwaje serikali itoe cheki ghushi?

Haya ni baadhi tu ya masuala ambayo yameibuliwa mtandaoni bila majibu.

Tunamwomba Gavana Wakujaa au wahusika wake serikalini wachukue muda kuchambua masuala haya na mengine ambayo hatujataja ili kuonyesha kama kweli Mwachere Shuma haelewi anachoandika.

Tukipata majibu, tutaomba msamaha na pengine tutaanza kuona mema ya serikali na kuwapongeza hata mara moja moja.

Mwisho

Kwaela News Network

Leave a Comment
Share
Published by
Kwaela News Network

Recent Posts

TAITA TAVETA: SEVEN DAYS HAVE ELAPSED — HAS SENATOR KAJWANG SENT WAKUJAA’S GOVERNMENT FILES TO EACC?

  By Kwaela News Network (KNN) | Governance & Accountability The seven-day ultimatum issued to…

17 hours ago

THE ERA OF POLITICAL EUPHORIA IN TAITA TAVETA COUNTY IS OVER

  The days when political party waves and symbolism single-handedly determined election outcomes in Taita-Taveta…

1 day ago

TAITA TAVETA: CAN THE DCI CRACK THE NUT? DORCAS MLGHU’S PUBLIC OUTBURST PUTS COUNTY EXECUTIVE UNDER FRESH PRESSURE

  The growing controversy surrounding the financial management of Taita Taveta County has taken another…

2 days ago

THE GOVERNOR DISCOVERS FISCAL DISCIPLINE — FOUR YEARS TOO LATE?

  Perhaps one of the most ironic moments of Governor Andrew Mwadime's appearance before the…

3 days ago

NDARA B LAND DISPUTE: 63 RESIDENTS SERVED WITH THREE-MONTH EVICTION NOTICE FOLLOWING COURT RULING

Affected families in Mlambenyi, Golani and Mto Mwagodi face a February 2027 deadline as the…

3 days ago

THE WRONG TIME: GOVERNOR WAKUJAA’S DEFENCE

During a Senate Public Finance Committee meeting, Taita Taveta Governor Andrew Mwadime, popularly known as…

5 days ago