Kuna tofauti kubwa kati ya kuwasaidia wananchi na kuwazoesha wananchi kutegemea vijisadaka vya kisiasa.
Kwa miaka mingi, tumeshuhudia mamilioni ya fedha za umma yakigawanywa katika miradi midogo midogo kwa jina la empowerment: bursary ya elfu mbili, viti vichache, hema hapa, sufuria pale, na misaada mingine inayotoweka haraka kuliko ilivyotolewa.
Lakini baada ya hapo, tunabaki na swali moja:
Mtoto anapewa bursary ya Sh2,000 lakini anaenda katika shule isiyo na maktaba, mabweni hayatoshi, dining hall haipo, paa linavuja na walimu hawatoshi.
Mama anapewa sufuria, lakini hana maji ya uhakika.
Kijana anapewa fedha kidogo za “empowerment”, lakini hana barabara, umeme, soko au mazingira ya biashara yanayoweza kumsaidia kujitegemea.
Hapo ndipo tunapaswa kuanza kufikiria upya.
Serikali inapaswa kuweka msingi wa maendeleo:
Maji. Afya. Umeme. Barabara. Shule. Masoko. Miundombinu ya uzalishaji.
Mwananchi naye akipata mazingira hayo, anaweza kupambana kutafuta mahitaji yake madogo—kununua hema, viti, sufuria, kulipa karo, kuanzisha biashara au kuboresha maisha ya familia yake.
Huo ndio uwezeshaji wenye maana.
Sio mfumo ambao kiongozi anajenga utegemezi kwa kugawa vijisenti huku akipata sifa za kisiasa.
Hoja hii inakuwa muhimu zaidi tunapozungumzia Mzima Phase Two.
Kwa miaka mingi, wananchi wa Taita Taveta wamekuwa wakisikia ahadi za mradi huu mkubwa wa maji. Gharama inayotajwa imefikia takribani Sh42 bilioni, lakini wananchi bado wanaendelea kuishi na uhaba wa maji.
Kwa nini tusifikirie utekelezaji wa mradi kwa awamu?
Ikiwa mradi mzima hauwezi kujengwa mara moja, serikali inaweza kuanza na maeneo yenye uhitaji mkubwa—kwa mfano kuhakikisha Voi na maeneo mengine muhimu yanapata maji ya uhakika—kisha kupanua mfumo hatua kwa hatua.
Wananchi hawahitaji kusubiri mradi mzima ukamilike ndipo waanze kupata maji.
Wanaweza kupata maji leo, wakati serikali ikiendelea kujenga kesho.
Hii ndiyo hoja ambayo Mheshimiwa Mwashako amekuwa akiibua: kupunguza miradi midogo midogo isiyobadilisha maisha ya wananchi na kuelekeza nguvu na rasilimali kwenye miradi mikubwa yenye athari pana.
Na katika suala la maji, hoja hiyo inahitaji mjadala wa wazi wa wananchi.
Vindo Sports Stadium inaweza kuwa na umuhimu wake. Barabara zina umuhimu. Reli ya Voi–Taveta ina umuhimu. Nyumba za gharama nafuu zina umuhimu.
Lakini mwananchi anayelala bila maji hawezi kunywa stadium.
Huwezi kupika kwa reli.
Huwezi kuoga kwa barabara.
Ndiyo maana swali si kama miradi hiyo ni mibaya.
Swali ni:
Ni mradi gani unaopaswa kupewa kipaumbele kwanza?
Kwa Taita Taveta, maji yanapaswa kuwa katika kilele cha ajenda.
Kwa sababu maji ni afya, maji ni usafi, maji ni kilimo, maji ni biashara, maji ni heshima ya maisha ya mwananchi.
Taita Taveta haiwezi kujenga uchumi wa kisasa kwa kutegemea handouts na miradi ya vijisenti.
Tunapaswa kuanza kuuliza viongozi wetu maswali magumu:
Umejenga nini kitakachobaki baada yako?
Je, umeacha maji ya uhakika?
Je, umeboresha shule?
Je, umejenga kituo cha afya kinachofanya kazi?
Je, umefungua eneo la uzalishaji?
Je, umeunganisha wananchi na barabara na umeme?
Au umeacha tu orodha ndefu ya watu uliowahi kuwapa Sh2,000?
Hapo ndipo tunapaswa kubadilisha siasa zetu.
Kutoka kwa siasa za kugawa kidogo kidogo kwenda kwa siasa za kujenga kikubwa kikubwa.
Kutoka kwa utegemezi kwenda kwa uwezeshaji wa kweli.
Kutoka kwa “ChuruChuru Projects” kwenda kwa miradi inayobadilisha maisha ya kizazi kizima.
Maendeleo mengine yanaweza kufuata.
By Kwaela News Network (KNN) | Governance & Accountability The seven-day ultimatum issued to…
The days when political party waves and symbolism single-handedly determined election outcomes in Taita-Taveta…
The growing controversy surrounding the financial management of Taita Taveta County has taken another…
Perhaps one of the most ironic moments of Governor Andrew Mwadime's appearance before the…
Affected families in Mlambenyi, Golani and Mto Mwagodi face a February 2027 deadline as the…
During a Senate Public Finance Committee meeting, Taita Taveta Governor Andrew Mwadime, popularly known as…
View Comments